29 Agosti 2021 - 11:20
Waasi wa ADF waua watu 15 huko Beni, DRC

Waasi wa kundi la ADF wameua raia 19 wilayani Beni, katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kwa mujibu wa taarifa mauaji hayo yalitokea siku ya Ijumaa ambapo baadhi ya miili imepatikana siku ya Jumamosi kufuatia hujuma ya waasi hao wa ADF katika kijiji cha Kasanzi.

Kiongozi wa kijiji hicho Kakule Kalunga, amesema watu hao 19 waliuawa kwa kuchomwa visu na wengine kupigwa risasi, huku nyumba zao zikichomwa moto.

Gavana wa zamani wa jimbo la Kivu Kaskazini Carly Nzanzu Kasivita kwenye ukarasa wake wa Twitter ameandika kuwa nyumba 13  pia zimeteketezwa moto katika hujuma hiyo.

Mwezi Mei Tshisekedi alitoa amri kwa jeshi na polisi ya nchi hiyo kuchukua jukumu la kuendesha mzingiro katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyio yaliyokumbwa na machafuko na mauaji ya mara kwa mara ya magenge ya waasi.

Licha ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutangaza mzingiro wa mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini, lakini mauaji ya raia yangali yanaendelea. 

Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, mbali na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi. 

Eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa lina utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.

342/